WELCOME ALL

Gonga Hapa.

Monday, August 16, 2010

Ngeleja: Tatizo la Lindi Mtwara ni la kiufundi

WELCOME TO KUNAMBI BLOG!!!

Ngeleja: Tatizo la Lindi Mtwara ni la kiufundi


Saturday, 29 May 2010 09:11

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja jana alitoa ufafanuzi wa tatizo la umeme kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara akisema kuwa linatokana na matatizo ya kiufundi na si mvutano kati ya Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni binafsi ya Artumas.

Waziri Ngeleja jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa Tanesco imepanga kuiikabidhi Artumas kazi ya kusambaza umeme kwenye mikoa hiyo ifikapo Juni mwaka huu. “Kama kuna tatizo la umeme katika mikoa hii ni technical problem (tatizo la kiufundi) na halihusiani na makabidhiano," alisema Waziri Ngeleja kwenye mkutano na waandishi wa habari.

"Kilichokwamisha makabidhiano hayo ni kutokamilika kwa ujenzi wa miundombinu katika baadhi ya maeneo. Kwa hiyo badala ya makabidhiano kufanyika mwezi Mei, sasa yatafanyika Juni.” Alisema miudombinu hiyo ni pamoja na ile inayotoka Tandahimba kwenda Masasi, pamoja na ile inayokwenda Msimbati. Alisema baada ya kukamilika kwa miundombinu hiyo, Tanesco watakabidhi jukumu la usafirishaji na usambaza umeme kwa Artumas.

Ngeleja, ambaye wizara yake inakuwa kwenye kiti moto inapofikia matatizo ya umeme, alisema katibu mkuu wa wizara hiyo yuko katika mikoa hiyo ili kuhakikisha kazi inafanyika kama ilivyopangwa. Jana vyombo vya habari viliripoti kuwa mikoa hiyo ipo katika hatari ya kukosa umeme kwa muda mrefu ujao baada ya kuibuka kwa mvutano kati ya Tanesco na Artumas kuhusu kutoa huduma hiyo. Kwa mujibu wa vyombo hivyo, mvutano huo uliibuka baada ya Artumas, iliyoingia mkataba na Tanesco Desemba mwaka 2008 wa kuzalisha, kusambaza pamoja na kutoa huduma ya umeme wa gesi katika mikoa hiyo, kushindwa kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, mkataba huo ulitaka Artumas kupitia kampuni tanzu ya Umoja Light kuanza kutoa huduma ya umeme Machi mwaka huu, lakini ikashindwa kutokana na kudaiwa kukosa fedha, vifaa pamoja na wataalamu. Kutokana na hali hiyo, Tanesco na Umoja Light walikubaliana tena kuwa hadi kufikia Mei 30 mwaka huu, Tanesco wawe wameshaondoka katika mikoa hiyo.


Kutokana na makabaliano hayo, Tanesco ililazimika kutoa ilani ya kuwahamisha wafanyakazi wake zaidi 120 kwenda mikoa mingine. Lakini taarifa hizo zilisema Mei 21 mwaka huu watendaji wa Umoja Light waliitisha kikao cha dharura na watendaji wa Tanesco na kuomba kuongeza muda hadi Desemba mwaka huu.

No comments: