WELCOME ALL

Gonga Hapa.

Thursday, October 13, 2011

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA Ofisi ya Waziri Mkuu TUME YA KUDHIBITI UKIMWI TANZANIA

BOHARI Kuu ya Dawa nchini (MSD) imesema idadi kubwa ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs) kwenye maghala yake zimekwisha muda wa matumizi na moja ya sababu ikiwa ni kuingizwa kwa dawa hizo na wafadhili bila kuzingatia mahitaji.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Joseph Mgaya aliieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi Dar es Salaam jana kuwa, Tanzania haina tatizo la dawa hizo za kurefusha maisha kwa sasa, ingawa nyingi zilizopo hazifai tena.

Akifafanua, Mgaya alisema tatizo hilo linatokea zaidi kwa ARVs za fungu la pili, zinazoletwa na wafadhili kutoka nje, maalumu kwa wagonjwa wa Ukimwi ambao virusi vinavyoshambulia kinga zao za mwili vimeshindwa kupozwa na dawa za fungu la kwanza.

“Dawa hizi tunazitegemea kutoka kwa wafadhili pekee kwa sababu Serikali haihusiki kuzinunua, zinaletwa kwetu kama msaada hasa na Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kusaidia Mapambano dhidi ya Ukimwi (PEPRAR) kwa wagonjwa ambao virusi vinavyowashambulia ni sugu.

“Kwa kweli asilimia kubwa ya dawa hizi tulizonazo sasa zimeharibika na tumegundua sababu mbalimbali zinazochangia hali hiyo, kuwa ni pamoja na kuletwa kwa wingi bila kuzingatia mahitaji, kukosekana kwa kemikali za kupima mwendelezo wa CD4 (aina ya vitendanishi) kwa wagonjwa walioanza kutumia ARVs,” alisema Mgaya.

Sababu nyingine aliyoitaja ni kukosekana kwa fedha za kukomboa dawa hizo kutoka bandarini, mara zinapowasili kutoka nje, kutokana na utaratibu uliowekwa na Serikali unaohitaji hatua nyingi ili kupata fedha kwa ajili ya shughuli kama hiyo. Hali hiyo, alisema imesababisha dawa hizo zianze kupungua uhai wake kabla hata ya kuingia kwenye maghala hayo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Ugavi wa MSD, Heri Mchunga aliiambia Kamati hiyo kuwa, pamoja na sababu hizo, kumekuwa na utaratibu usiofaa wa Serikali kubadili miongozo ya aina za dawa zinazofaa kutumika kwa wagonjwa hao, bila kuzingatia uwepo wa dawa za awali katika bohari hiyo.

Hata hivyo, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Joseph Muhume alifafanua kwamba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii haiwezi kubadilisha miongozo ya matumizi ya dawa ghafla, bila utaratibu na bila maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na kwamba, wanaofanya hivyo ni wahusika katika vituo vya afya wenyewe.

“Ni kweli kuna tatizo la wagonjwa kubadilishiwa miongozo ya dawa kiholela. Wakati wanapaswa kutumia hizo za kundi la pili, unakuta wamehamia kwenye dawa nyingine na kuzifanya zilizopo kukosa watumiaji na kuharibika, huku hali halisi ya uhitaji ikiendelea kuwepo. Serikali inalifanyia kazi suala hili,” alisema Muhume.

Alisema Serikali inatekeleza wajibu wake wa kuhakikisha kuwa dawa zote zinazoingia nchini zina asilimia 80 ya uhai, ikiwa na maana kuwa, asilimia 20 pekee ya uhai huo ndio unayoruhusiwa kisheria kupotea njiani.

Wakati huo huo, MSD imekiri kuwepo kwa tatizo la vitendanishi vinavyosaidia kugundua endapo mpimwaji ana VVU au la, na kusema tatizo hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa fedha za kuvinunulia huku utegemezi wa fedha kutoka kwa wafadhili ukiwakwamisha kutokana na kutozituma kwa wakati.

Mgaya alisema, mahitaji ni makubwa kuliko uwezo wao wa kununua vitendanishi hivyo kutokana na kupewa mgawo mdogo sana wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa nyingine.

“Kwa mfano katika mwaka wa fedha 2011/2012, tuliomba shilingi bilioni 158 kwa ajili ya kufanya ununuzi huo, lakini tukatengewa shilingi bilioni 78 tu. Changamoto hii ni kubwa sana katika kutekeleza mapambano dhidi ya Ukimwi na kinachokwaza zaidi ni utegemezi wetu kwa wafadhili katika kuuendeleza mradi wa Ukimwi,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa MSD.

Hata hivyo, Muhume alijibu kuwa Serikali haina budi kuendelea kuwategemea wafadhili hao kwa sababu ni masikini na kwamba inachokitenga ndio uwezo wake, licha ya kujua ukubwa wa tatizo.

Muhume aliieleza kamati hiyo kuwa baada ya kujulishwa tatizo hilo na MSD, Serikali ilifanya jitihada na kuingiza nchini vitendanishi 34,000 vitakavyotosha kuihudumia nchi kwa miezi minne pekee, huku ikisubiri kuletewa vingine kwa ajili ya kupima CD4, vinavyotarajiwa kufika nchini mwishoni mwa mwezi huu.

“Tunafanya tuwezalo kuhakikisha kuwa hadi mwisho wa Novemba tatizo la dawa za kupima VVU linakwisha kabisa,” alisema na kuelezwa na wabunge kuwa akiwa mwakilishi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii anapaswa kuifikishia Serikali ujumbe wa kufanya uamuzi wa kujitegemea katika vita dhidi ya Ukimwi vinginevyo wananchi wataangamia.

No comments: