Wasanii maarufu wa Orijino Komedi na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’ na bendi yake ya Machozi wanatarajiwa kutumika kutunisha mfuko utakaofanikisha Siku ya Utalii Duniani, ambayo kitaifa itafanyika mkoani hapa. Zaidi ya Sh milioni 120 zimekadiriwa kutumika kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe hiyo itakayofanyika kwa wiki nzima kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 4, mwaka huu.
Mratibu wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe hizo, Fidiah Nakamendu alisema jana kwenye kikao cha maandalizi kwamba sherehe hizo zitafanyika nje kidogo ya Manispaa ya Iringa katika Kijiji cha Nduli, karibu na Uwanja wa Ndege wa Nduli. Alisema wasanii hao watafanya maonyesho yao katika mabonanza yatakayoandaliwa baadaye mjini Iringa. Alitaja mikakati mingine itakayofanikisha upatikanaji wa fedha hizo kuwa ni pamoja na kutuma barua za maombi ya michango kwa wadau mbalimbali wa utalii kama asasi za kiserikali na zisizo za kiserikali.
Mikakati mingine ni pamoja na kuandaa chakula cha hisani na kufanya tamasha la kitamaduni la chakula, mavazi na ngoma za asili. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Mrisho ambaye ni Mwenyekiti wa sherehe hizo, ameagiza kamati hiyo ifungue akaunti maalumu ya sherehe itakayokuwa na wajumbe wawili kutoka sekta ya umma na wengine wawili kutoka sekta binafsi na kuupongeza uamuzi wa kamati kufanyia sherehe hizo karibu na Uwanja wa Ndege wa Nduli kwani utaongeza changamoto katika kuendeleza utalii wa Mkoa wa Iringa. Kulingana na waandaaji, wakati wa sherehe hizo wageni watapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo mkoani hapa kwa gharama nafuu, pia kutakuwa na maonyesho ya vikundi mbalimbali vya burudani.
No comments:
Post a Comment